Michezo

Bandari FC: Kikosi Kitakachovaana na Yanga

Bandari FC: Kikosi Kitakachovaana na Yanga

Bandari FC Inayoivaa Yanga Leo

Bandari Football Club, inayotambulika pia kama “Dockers”, ni moja ya klabu kongwe na maarufu zaidi nchini Kenya yenye maskani yake jijini Mombasa. Klabu hii ilianza safari yake mwaka 1960 ikijulikana kama LASCO kabla ya kubadilishwa jina kuwa Cargo. Baadaye, mnamo mwaka 1985, iliunganishwa na kikosi cha Kenya Ports Authority (KPA) na ndipo ikazaliwa Bandari FC tuliyo nayo sasa.

Bandari FC Msimu Uliopita

Msimu uliopita, Bandari FC ilimaliza katika nafasi ya nane kwenye Ligi Kuu ya Kenya ikiwa na pointi 44. Hata hivyo, walishindwa kushinda katika mechi tano za mwisho, wakitoa sare nne dhidi ya Posta Rangers (1-1), Mathare United (0-0), AFC Leopards (0-0), Mara Sugar na kupoteza 1-0 dhidi ya Polisi waliotwaa ubingwa.

Historia ya Bandari FC

  • Chimbuko: Klabu hii ilianza mwaka 1960 kwa jina la LASCO, baadaye ikawa Cargo kabla ya kuungana na Kenya Ports Authority (KPA) mwaka 1985 na kuunda Bandari ya sasa.
  • Safari ya ligi: Ilipanda na kushuka mara kadhaa lakini ilirejea kwa kishindo, ikimaliza ya pili msimu wa 2017 na 2018.
  • Tuzo: Ilitwaa ubingwa wa SportPesa Super Cup 2018, ikapata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
  • Mashindano ya kimataifa: Iliwahi kuwatoa Al Ahly Shendi ya Sudan na US Ben Guardane ya Tunisia kwa sare za ugenini.
  • Changamoto: Ilifutwa mwaka 1999 lakini ikarejeshwa 2004 na kupanda hadi Ligi Kuu kwa haraka.
  • Kombe la Kenya: Iliwahi kufika fainali mwaka 1986 lakini ikapoteza dhidi ya Gor Mahia.

Kikosi cha Bandari FC

Kikosi cha sasa cha Bandari kina wastani wa umri wa miaka 26.3, kikiwa na wachezaji wengi wa ndani na asilimia 25 ya wachezaji wa kigeni. Baadhi ya nyota wao ni:

  • Joseph Okoth
  • Andrew Juma
  • Edward Satulo
  • Siraj Mohammed
  • Michael Sunday Apudo
  • Jackson Dwang (kiungo kutoka Sudan Kusini)
  • William Wadri (mshambuliaji hatari kutoka Uganda, 29)

Wachezaji hawa wanatarajiwa kuibeba Bandari dhidi ya Yanga kutokana na uzoefu wao wa ligi ya Kenya na michuano ya kimataifa.

Kocha Mkuu wa Bandari FC

Ken Odhiambo ndiye kocha mkuu wa Bandari FC tangu Julai 2024, akirithi mikoba ya John Baraza. Odhiambo, ambaye pia ni msaidizi wa kocha wa Harambee Stars, Benni McCarthy, yupo katika ukurasa wake wa tatu na Bandari. Anasaidiwa na John Baraza, aliyewahi kushika mikoba ya timu hiyo baada ya Twahir Muhiddin kuondolewa.

Lengo la Odhiambo ni kuirudisha Bandari kwenye hadhi ya juu ya soka la Kenya na kutumia mechi dhidi ya Yanga kama kipimo cha maandalizi ya msimu mpya.

Mashabiki wa Yanga, maarufu kama Wananchi, leo wanashuhudia kilele cha tamasha lao kubwa la kila mwaka. Katika tamasha hilo, Yanga itacheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Bandari FC ya Kenya, ikiwa ni kipimo cha wachezaji wapya waliotua Jangwani akiwemo Celestin Ecua (Zoman FC), Mohamed Doumbia (Majestic), Balla Moussa Conte (CS Sfaxien), Offen Chikola (Tabora United), Lassine Kouma (Stade Malien), Andy Boyeli (Sekhukhune) na Mohammed Hussein (Simba).