Ebitoke Awashukuru Mashabiki kwa Upendo na Maombi
DAR ES SALAAM – Msanii maarufu wa vichekesho, Annastazia Exavery ‘Ebitoke’, ameonyesha shukrani kubwa kwa mashabiki wake waliompa moyo, maombi na sapoti alipokuwa akipitia kipindi kigumu cha changamoto za afya ya akili.
Changamoto Alizopitia
Kupitia taarifa yake, Ebitoke alifunguka kuwa alipitia hali ngumu iliyotokana na matatizo aliyodai yalihusiana na kulogwa, jambo lililomwathiri kisaikolojia. Alisema maombi na sapoti za mashabiki wake vilikuwa msaada mkubwa katika kumvusha kwenye changamoto hizo.
“Ningependa kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa moyo mmoja mashabiki wangu wote na kila mmoja alieguswa na safari yangu. Upendo wenu mkubwa, maombi yenu ya dhati na sapoti yenu ya hali ya juu vimenitia moyo sana wakati nilipokuwa napitia changamoto ya afya ya akili,” alisema Ebitoke.
Moyo Mpya na Hatua Anazochukua
Ebitoke aliongeza kuwa kila sala na ujumbe wa faraja alioupokea ulimfanya ajisikie kama sehemu ya familia kubwa yenye upendo. Kwa sasa anasema anaendelea vizuri kwa neema ya Mungu na ana matumaini mapya ya kurejea katika hali yake ya kawaida, huku akisisitiza kuwa nguvu alizonazo zimetiwa na mashabiki wake.
Umaarufu Wake
Ebitoke ni miongoni mwa wasanii wa vichekesho waliopata umaarufu mkubwa kupitia mitandao ya kijamii na vipindi vya televisheni kutokana na ucheshi wake wa kipekee na nafasi yake katika tasnia ya burudani.
Shukrani zake zimeonesha mshikamano wa mashabiki wake na kuonyesha namna sapoti ya kijamii inavyoweza kuwa tiba muhimu kwa msanii anapokumbana na changamoto binafsi.