Udahili Vyuo Vikuu 2025/2026: Awamu ya Kwanza Yafungwa, Awamu ya Pili Yaendelea
Kukamilika kwa Awamu ya Kwanza ya Udahili 2025/2026
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza kukamilika kwa Awamu ya Kwanza ya udahili wa Shahada ya Kwanza kwa mwaka wa masomo 2025/2026. Majina ya waliodahiliwa yametolewa na vyuo husika kote nchini.
Katika awamu hii, jumla ya waombaji 146,879 walituma maombi ya kujiunga katika vyuo 88 vilivyoidhinishwa kudahili wanafunzi. Idadi ya programu zilizothibitishwa ni 894, ikilinganishwa na 856 mwaka uliopita, ongezeko la programu 38. Nafasi za udahili zimeongezeka hadi 205,652, kutoka 198,986 mwaka 2024/2025, ongezeko la nafasi 6,666 sawa na asilimia 3.3.
Kwa jumla, waombaji 116,596 (sawa na 79.4%) wamepata udahili katika vyuo walivyoomba. Idadi hii inatarajiwa kuongezeka zaidi kupitia Awamu ya Pili ya udahili.
Waombaji Waliochaguliwa Zaidi ya Chuo Kimoja
Waombaji waliodahiliwa katika vyuo zaidi ya kimoja wanapaswa kuthibitisha chuo wanachokichagua kati ya 03–21 Septemba 2025. Uthibitisho unafanyika kwa kutumia namba ya siri iliyotumwa kupitia SMS au barua pepe.
Kwa wale ambao hawajapokea ujumbe huo kwa wakati, wanashauriwa kuingia kwenye mifumo ya udahili ya vyuo husika na kuomba namba ya siri ili kujithibitisha. Orodha ya majina ya waliodahiliwa katika zaidi ya chuo kimoja inapatikana kupitia tovuti ya TCU.
Kufunguliwa kwa Awamu ya Pili ya Udahili 2025/2026
TCU imetangaza kuwa Awamu ya Pili ya udahili imefunguliwa kuanzia 03–21 Septemba 2025. Waombaji ambao hawakudahiliwa au hawakutuma maombi katika awamu ya kwanza wanahimizwa kutumia fursa hii.
Vyuo vimeelekezwa kutangaza programu ambazo bado zina nafasi, huku waombaji wakitakiwa kuzingatia kalenda ya udahili inayoonekana kwenye tovuti ya TCU.
Wito kwa Waombaji wa Udahili
TCU inawakumbusha waombaji wote kuwa masuala yote ya udahili na uthibitisho yafanyike moja kwa moja kwenye vyuo husika. Vyuo vyote vimeelekezwa kushughulikia changamoto zinazoweza kujitokeza kwa haraka na kwa mujibu wa miongozo ya TCU.
Imetolewa na:
Prof. Charles D. Kihampa
Katibu Mtendaji, TCU