Michezo

Yanga Yaanza Ushirikiano wa AI na BlackBird

Yanga Yaanza Ushirikiano wa AI na BlackBird

Yanga Yaanza Ushirikiano wa Kiteknolojia ya AI

Klabu ya Young Africans (Yanga SC) imetangaza rasmi kuingia mkataba wa kipekee na kampuni ya BlackBird kutoka Rotterdam, Uholanzi, kwa ajili ya kutumia teknolojia ya Artificial Intelligence (AI). Mfumo huu mpya utaisaidia klabu hiyo kukusanya na kuchambua taarifa muhimu za wachezaji wake.

Yanga Klabu ya Kwanza Afrika

Rais wa Yanga, Eng. Hersi, amesema makubaliano hayo yaliyosainiwa Septemba 11, 2025, yanaifanya Yanga kuwa klabu ya kwanza barani Afrika kuingia mkataba wa aina hii. Akizungumza wakati wa utiaji saini, Hersi alisema mfumo wa AI utaboresha namna klabu inavyosimamia data za wachezaji na kuongeza ufanisi wa kiufundi.

Kauli ya BlackBird

Mkurugenzi wa kampuni ya BlackBird, Thim van der Weijden, alieleza kufurahishwa na ushirikiano huo akisema:

“Tunayofuraha kubwa sana kushirikiana na klabu ya Yanga. Tulichagua Yanga kwa sababu ni moja ya klabu kubwa barani Afrika na tumevutiwa na mchakato wao wa mabadiliko. Mfumo huu wa kiteknolojia utaiwezesha Yanga kuendana na kasi ya teknolojia ya kisasa.”

Umuhimu kwa Mustakabali wa Yanga

Kupitia mkataba huu, Yanga inaimarisha nafasi yake kama klabu inayoongoza katika mageuzi ya kisoka barani Afrika. Uwekezaji katika AI unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwenye ufuatiliaji wa takwimu za wachezaji, maamuzi ya kiufundi, na kuongeza ushindani wa klabu kimataifa.